HATIMAYE kazi ya kutandika lami katika barabara ya daraja la Kibonde Mzungu inayofanywa na kampuni ya ujenzi MECCO kutoka Dar es Salaam imekamilika.
Hatua hiyo imefikiwa juzi Jumapili ambapo waandishi walioitembelea barabara hiyo walishuhudia shughuli ikiendelea hadi kiza kikiingia kuruhusu taa zilizowekwa katikati ya daraja hilo kuwaka na kupendezesha mandhari ya eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo hilo, msimamizi wa ujenzi wa barabara hiyo kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mhandisi Cosmas Masolwa, alieleza kufurahishwa na hatua hiyo huku akisifia utaalamu wa Mkandarasi kwa kukidhi kiwango kinachotakiwa.
Alisema kwa ujumla, ujenzi huo umefikia asilimia 90, na kazi iliyobaki kwa sasa ni kukamilisha njia za waendao kwa miguu.
“Ujenzi unajumuisha madaraja matatu, njia mbili pacha zenye urefu wa mita 460 kwa ajili ya vyombo vya moto na zile za waendao kwa miguu pamoja na taa mnazoziona ambazo zimewekwa leo zinazowaka kila kiza kinapoingia,” alifafanua.
Aidha alisema kukamilikka kwa ujenzi wa daraja hilo kunatoa matumaini ya kukoma tatizo la kujaa na kutuwana maji kwenye bonde hilo, hali iliyokuwa ikileta maafa ya watu na vyombo kuzama na kusababisha vifo.
Hata hivyo, alisema serikali imeamua kumuongezea Mkandarasi kazi nyengine ya kuunganisha kwa lami kilomita 1.02 hadi kufikia kituo cha Polisi Fuoni kwa gharama ya shilingi bilioni 3.8 ikichanganywa na shilingi 117,000,000. zilizobaki katika bajeti ya awali ya shilingi bilioni 4.08.
Msimamizi huyo alieleza kuwa hatua hiyo imelenga kulipa eneo hilo mvuto mpya utakaolifanya lipendeze, kwani dhamira ya serikali ni kuzitengeneza barabara zote kwa kiwango kizuri kama hicho cha Kibonde Mzungu.
“MECCO imejitahidi kufanya kazi hii kwa namna ilivotakiwa na serikali, mtu akiiona tu anajua kuwa barabara hii ni nzuri. Ufanisi huu unaongeza imani yetu na nafasi kwa kampuni hii kupata kazi nyengine hapo baadae,” alieleza.